Ndugu Wadau wa Kampeni;
Ndugu Watanzania Wenzangu;
Mabibi na Mabwana;
Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kufika siku hii ya leo; na kwa kutujalia pumzi na nguvu kwa kipindi chote cha mwaka huu tangu tulipozindua Kampeni hii ya Kuinua Maadili Kitaifa Januari hadi leo Disemba 2017.
Pia, nichukue fursa hii kuwashukuru wote walio ndani na nje ya nchi kwa kushiriki kampeni hii.
Vilevile, niwashukuru sana na kuwapongeza; wadau wote kutoka ndani na nje ya nchi waliojitoa kwa hali na mali kuchangia mahitaji ya kampeni hii. Wameonyesha moyo wa uzalendo wa hali ya juu sana kwani kuunga mkono suala la maadili ni kuunga mkono sekta zote za maandeleo ya jamii katika Taifa. Kitendo hiki kimeonyesha unyeneyekevu na upendo wa dhati kwa taifa letu. Tunaamini mbegu ya mwenendo kama huo wa moyo uzalendo wa kweli ni uthibitisho kuwa; pamoja na tatizo kubwa la mmomonyoko wa maadili uliokithiri nchini na duaniani kwa ujumla, bado nyumbani kwetu Tanzania tuna watu wenye maadili mema ambao wakithaminiwa na kuenziwa; tutaweza kulijengea taifa mfumo hai na kuliondoa katika mfumo mfu usiojali utu, upendo na umoja wa kitaifa.
Na mwisho ila kwa umuhimu wa pekee, ninawashukuru ninyi nyote mlioacha shughuli zenu na kushiriki katika maadhimisho haya siku ya leo. Mwenyezi Mungu awabariki sana na kuwajaalia maisha marefu yenye tija na furaha.
Ndugu Watanzania Wenzangu;
Tarehe 14 Januari, 2017 Mwanaharakati Mayrose Kavura Majinge kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo waishio Marekani waliandaa na kuzindua Kampeni Maalum ya Kuinua Maadili Kitaifa ambayo leo tunaadhimisha kilele cha Awamu ya kwanza.
Lengo Kuu la Kampeni hii ni Kuinua maadili mema kwa ajili ya kujenga mfumo bora katika kuendesha maisha yetu ya kila siku.
Kampeni hii iliendeshwa kwa njia ya Midahalo, Shindano la Hoja, Usaili na tafakari kwa kutilia mkazo maelezo ya kitabu cha Kampeni kiitwacho: “Chombo Muhimu kwa Maendeleo Yako”
Kauli Mbiu ya Kampeni: “Maadili mema na mfumo bora katika jamii vinaanza na mimi na wewe, tujielekeze kwenye ukweli huu tujenge maisha yenye tija”
Ndugu Watanzania wenzangu;
Kampeni hii iliendeshwa kwa kutumia vyombo vya habari kwa lengo la kuwafikishia ujumbe Watanzania wote waishio ndani na nje ya nchi yetu.
Vyombo vya habari vilivyojitoteza kusambaza ujumbe wa kampeni hii ni mitandao ya kijamii zikiwemo Blogs ambapo tuna blog ya kampeni hii: www.maadilikitaifa.blogspot.com ; Youtube; WhatsApp; Emails; Facebook; twitter; Instagram, pamoja na usambazaji wa kitabu cha kampeni sehemu mbalimbali nchini.
Tunawashukuru sana wanahabari na wadau wote walioshiriki katika awamu ya kwanza ya kampeni hii muhimu kwa mstakabali wa Maendeleo ya Taifa letu.
Ushiriki wenu umeonyesha moyo wa uzalendo.