Tuesday, December 19, 2017

KILELE CHA AWAMU YA KWANZA YA KAMPENI YA KUINUA MAADILI KITAIFA TAREHE 10 DESEMBA 2017

Ndugu Wadau wa Kampeni;
Ndugu Watanzania Wenzangu;
Mabibi na Mabwana;

Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kufika siku hii ya leo; na kwa kutujalia pumzi na nguvu kwa kipindi chote cha mwaka huu tangu tulipozindua Kampeni hii ya Kuinua Maadili Kitaifa Januari hadi leo Disemba 2017.

Pia, nichukue fursa hii kuwashukuru wote walio ndani na nje ya nchi kwa kushiriki kampeni hii.
Vilevile, niwashukuru sana na kuwapongeza; wadau wote kutoka ndani na nje ya nchi waliojitoa kwa hali na mali kuchangia mahitaji ya kampeni hii. Wameonyesha moyo wa uzalendo wa hali ya juu sana kwani kuunga mkono suala la maadili ni kuunga mkono sekta zote za maandeleo ya jamii katika Taifa. Kitendo hiki kimeonyesha unyeneyekevu na upendo wa dhati kwa taifa letu. Tunaamini mbegu ya mwenendo kama huo wa moyo uzalendo wa kweli ni uthibitisho kuwa; pamoja na tatizo kubwa la mmomonyoko wa maadili uliokithiri nchini na duaniani kwa ujumla, bado nyumbani kwetu Tanzania tuna watu wenye maadili mema ambao wakithaminiwa na kuenziwa; tutaweza kulijengea taifa mfumo hai na kuliondoa katika mfumo mfu usiojali utu, upendo na umoja wa kitaifa. 
Na mwisho ila kwa umuhimu wa pekee, ninawashukuru ninyi nyote mlioacha shughuli zenu na kushiriki katika maadhimisho haya siku ya leo. Mwenyezi Mungu awabariki sana na kuwajaalia maisha marefu yenye tija na furaha.

Ndugu Watanzania Wenzangu;

Tarehe 14 Januari, 2017 Mwanaharakati Mayrose Kavura Majinge kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo waishio Marekani waliandaa na kuzindua Kampeni Maalum ya Kuinua  Maadili Kitaifa ambayo leo tunaadhimisha kilele cha Awamu ya kwanza.

Lengo  Kuu la Kampeni hii ni  Kuinua maadili mema kwa ajili ya kujenga mfumo bora katika kuendesha maisha yetu ya kila siku.

Kampeni hii iliendeshwa kwa njia ya Midahalo, Shindano la Hoja, Usaili na tafakari kwa kutilia mkazo maelezo ya kitabu cha Kampeni kiitwacho: “Chombo Muhimu kwa Maendeleo Yako”


Kauli Mbiu ya Kampeni: “Maadili mema na mfumo bora katika jamii vinaanza na mimi na wewe, tujielekeze kwenye ukweli huu tujenge maisha yenye tija”

Ndugu Watanzania wenzangu;
Kampeni hii iliendeshwa kwa kutumia vyombo vya habari kwa lengo la kuwafikishia ujumbe Watanzania wote waishio ndani na nje ya nchi yetu.
Vyombo vya habari vilivyojitoteza kusambaza ujumbe wa kampeni hii ni mitandao ya kijamii zikiwemo Blogs ambapo tuna blog ya kampeni hii: www.maadilikitaifa.blogspot.com ; Youtube; WhatsApp; Emails; Facebook; twitter; Instagram, pamoja na usambazaji wa kitabu cha kampeni sehemu mbalimbali nchini.
Tunawashukuru sana wanahabari na wadau wote walioshiriki katika awamu ya kwanza ya kampeni hii muhimu kwa mstakabali wa Maendeleo ya Taifa letu. 
Ushiriki wenu umeonyesha moyo wa uzalendo.


Katika kufikia lengo la kampeni hii; Kamati ya Kampeni ya Kuinua Maadili Kitaifa inatoa wito kwa Serikali kuwaangalia kwa jicho la uwezeshwaji wadau wa habari wote wakiwemo viongozi na wamiliki wa mitandao za kijamii ili kuwatia moyo na kuwawezesha kisera; hatimae waweze kufanya shughuli za kuielimisha jamii yetu kwa maadili, amani, umahiri na kwa uwigo mpana zaidi. Maana  hatuwezi kusema Taifa  linapiga hatua za kimaendeleo huku tukiwaacha wanahabari nyuma! Lazima tutambue kwamba Wanahabari wa aina zote ndio wahamasishaji wakuu wa maendeleo katika jamii. Kuwaacha nyuma, kuwagandamiza kwa namna yoyote, au kutotilia mkazo haki zao za msingi ni kutoyatilia mkazo maendeleo na kupoteza mwelekeo katika kuliletea taifa tija na maendeleo kwa ujumla.

Nawaalika; wanaharakati wenzangu; taasisi mbalimbali za maendeleo ya jamii; na watanzania wote wenye uwezo wa kutetea haki; tuamke, tuungane pamoja kwa ajili ya kuhakikisha kwamba; wanahabari wetu wote wanapata haki zao na wanathaminiwa na kuenziwa kwa ajili ya maslahi ya taifa letu!


Ndugu Watanzania Wenzangu;
Lengo la Kampeni hii litafikiwa hatua kwa hatua. 
Hivyo kilele cha kampeni hii ya awamu ya kwanza ni hatua mojawapo katika kufikia lengo kuu la kampeni hii.
Awamu ya pili ya Kampeni hii inaandaliwa kwa weledi mkubwa. Maandalizi yakikamilika; jamii itaarifiwa kwa ajili ya kuiunga mkono kwa maslahi ya Taifa zima. 
Ni muhimu kutambua kwamba; faida za kampeni ya kuinua maadili kitaifa niza kizazi na kizazi. Maana bila maadili hatuwezi kufikia maendeleo.

Ndugu Watanzania Wenzangu;
Maendeleo kwa maana ya maendeleo; ni maendeleo ya watu. Taifa haliwezi kusema limeendelea ikiwa watu wake waliowengi wanahangaika na hofu; hawana furaha wala heshima wamepoteza matumaini; ni watu masikini.
Maadili mema hujenga siasa safi, bidii katika kazi, hujenga maarifa, hujenga kujiamini na kuaminiwa; hujenga hadhi na heshima ya mtu na taifa kwa ujumla. Ni nyenzo mtambuka ya kuondoa umaskini. 
Kwa hiyo ni dhahiri kuwa; ili Taifa lolote lipate maendeleo lazima lijikite katika kuwekeza na kuimarisha rasilimali watu kimaadili. Maana taifa linalosimamia na kuthamini maadili ya watu wake hujenga nguvu za kiafya, kielimu,  kiuchumi, kiusalama na kidemokrasia.


Ndugu Watanzania Wenzangu;
Wakati nafuatilia umuhimu wa maadili katika maisha ya kila siku ya watu, nilikutana na  sheria inayojulikana kama Sheria Wote ya Mvuto/Kivutio (The Universal Law of Attraction). Sheria Wote ya Mvuto inasema kwamba; katika kuishi kwako, taratibu bila kujua, unajikuta umevutia maadili na fikra zako mfu kuendana na watu na mazingira yako. Hii ina maana kwamba kwa kila jambo la maisha yako umevutia, kwa namna wewe  mwenyewe ulivyo. Kama kuna kitu katika maisha yako, mahusiano yako, au kazi yako vinakufanya usiwe na furaha, unahitaji kuanza kubadilika ulivyo wewe, ili kwamba kuzuia kuvutia hao watu na hali iliyopo katika maisha yako.

Katika uchunguzi nilioufanya kupitia maendeleo ya watu, imeonekana kwamba; Sheria Wote ya Mvuto inaathari kubwa sana katika kuunda mfumo wa kijamii.
Hivyo ni muhimu sana kuitambua sheria hii na kuangalia namna ya kuithibiti ili kujenga mfumo mathubuti wa kuliwezesha taifa letu kuwa na watu wenye furaha.

Ndugu Watanzania Wenzangu;
Kampeni yetu hii inaonyesha mafanikio makubwa sana kwa mstakabali wa kujenga Taifa lenye tija kwa Watanzania wote. Mambo yaliyoelezwa na washiriki wa kampeni endapo yatafanyiwa kazi  yatalijengea Taifa mfumo hai; na kuliondolea mfumo mfu unaolifunika taifa kwa muda mrefu sasa.
Baadhi ya mambo yaliyojitokeza kutokana na michango ya washiriki ni kama yafuatayo:

1. Kwa upande wa Usaili, Ushauri na Maoni: 
Washiriki wa kampeni wameshauri kuwa; Suala la Maadili liwe somo la lazima katika ngazi zote yaani shuleni, kazini na nyumbani.
Washiriki wamependekeza kuwa; Viongozi wa ngazi zote wakiwemo wakubwa wote  kuanzia ngazi ya familia hadi taifa; wawe mstari wa mbele kuonyesha maadili kwa vitendo kwa kuwa wao ni vioo vya jamii
Washiriki wameshauri kuwa kitabu kilichotumika wakati wa Kampeni Kinachoitwa ‘Chombo Muhimu Kwa Maendeleo Yako” mikakati zaidi zitumike kiwafikie Watanzania wengi zaidi ili kisaidie kukuza mwamko wa maadili nchini petu.

2. Kwa upande wa Shindano la Hoja Juu ya Sifa Za Rais Bora wa Nchi Kama Tanzania:
Washiriki walikiri kwamba; kampeni imewakumbusha mambo mengi ya msingi kwa mfano kuhusu Ngao ya Taifa ambayo ni UHURU NA UMOJA. Baadhi walidai walishaisahau na wengine wengi walikiri kutoijua kabisa.
Katika Shindano hilo; Washiriki walionyesha kukubaliana na ile kauli iliyotolewa wakati wa uzinduzi wa Shindano la Hoja; kuwa; wakati wa uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani; Taifa lisiwaachie wanasiasa kupitia vyama  vyao watuchagulie DHUMUNI KUU LA KUONGOZA NCHI. Wakamuunga mkono Kiongozi wa Kampeni Bi. Mayrose Majinge kwamba; Dhumuni Kuu la chama chochote kinachotaka kuongoza Taifa, lilenge maslahi ya Watanzania wote, na sio ya chama cha siasa. 
Katika Shindano hilo Pia wadau waliunga mkono kuwa; suala la sifa za kiongozi mkuu wa nchi (Rais) ni muhimu ziboreshwe na kuwekwa wazi kwa Watanzania wote ili wakati wa uchaguzi mkuu ziweze kumsaidia mpiga kura kuainisha mgombea bora kwa maslahi ya Taifa na sio ya chama fulani cha siasa.


Ndugu Watanzania Wenzangu;
Katika mchakato wa kuchambua hoja zilizotolewa wakati wa Shindano Juu ya Sifa za Rais Bora wa Nchi Kama Tanzania.  Kamati ya Uchambuzi wa Shindano la Hoja  iliweza kuainisha sifa 12 za Rais bora wa nchi. Sifa hizo ni:
1. Awe Mtanzania mwenye umri kati ya miaka 40 hadi 55.
2. Awe ana elimu ya ngazi ya Shahada au zaidi
3. Awe mwenye upendo wa dhati kwa Taifa (Mzalendo). 
4. Awe mwadilifu katika mienendo yake tangu awali
5. Mwenye kukubali kukosolewa na kushauriwa
6. Awe anajali haki na usawa wa watu wake
7. Awe mwenye kuheshimu sheria na taratibu za kiuongozi
8. Ithibitike kuwa anachukia rushwa kutokana na rekodi zake za nyuma
9. Awe na kiona mbali na mwenye uwezo wa kubeba na kusimamia kwa weledi mkubwa mwelekeo wa maendeleo ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla
10. Awe na uwezo wa kujenga mahusiano mema ndani na nje ya nchi
11. Awe na uthubutu wa hali ya juu katika kutenda mambo. Na ithibitike kwa mienendo na matendo yake ya tangu awali kuwa ana umahiri zaidi wa kuweza kukabiliana na changamoto mbalimbali kwa weledi na heshima. 
12. Awe amewahi kushika nafasi ya kuiongoza jamii na athibitishe namna alivyowahi kutumia nafasi hiyo kwa kufuata diplomasia (sio mabavu) na heshima. 


Ndugu Watanzania Wenzangu;
Pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana katika Kampeni hii, pia tulikutana na changamoto mbalimbali. Hapa nitataja moja kubwa:
Changamoto kubwa iliyojitokeza ni hofu iliyotanda kwa walengwa wa Kampeni hii.
Tukumbuke kwamba walengwa wa kampeni hii ni watanzania wote.
Wakati tunaendesha kampeni tulikabiliana na hali ya hofu ilionekana kuwakumba Watanzania wengi na hivyo kusababisha ushiriki hafifu wa kampeni. Kuna baadhi ya watu walitutumia taarifa kuwa wanatamani kushiriki na kuwahamasisha wengine hasa kwenye shindano la hoja; lakini wanahofu ya kujieleza kwa uwazi kwenye umma kutokana na matukio yaliyosababisha hali ya sintofahamu yaliyotokea na yanayoendelea kutokea katika Taifa letu siku hizi.
Kutokana na hali ya hofu ikapelekea kanuni na taratibu za kushiriki Shindano la Hoja Juu ya Rais Bora kutoweza kufuatwa na hivyo kamati haikuweza kuwapata washindi wa shindano.Kutokana na hali hiyo zawadi zilizokuwa zimeandaliwa hazikuweza kutolewa hasa zile za fedha taslimu. 



Ndugu Watanzania Wenzangu;
Nchi yetu Tanzania imeripotiwa na World Happiness kwamba; sisi watu wake tumekuwa wa tatu duniani kwa kuishi bila furaha. Hii ni aibu na inasikitisha sana. Inaonyesha jinsi tulivyo na hali mbaya kimaisha. Maana hatuwezi kusema tunapiga hatua za kimaendeleo, wakati watu wetu hawana furaha. Hatuna budi kujitafakari upya na kuchukua hatua sitahiki. Maana kuishi ni kufurahi. 
Furaha ya mtu hutokana na hali yake ya kiafya, kiuelewa, kiuchumi, kiusalama na kidemokrasia katika maisha yake na ya wapendwa wake. 

Katika mataifa ambayo yana jamii yenye furaha, kwa mfano: mataifa ya Norway, Denmark, Switzerland, Finland, Canada na yote yaliyoainishwa kwa mujibu wa ripoti ya World Happiness, utagundua kwamba  katika mataifa hayo, watu wenye maadili huenziwa na kuthaminiwa sana, tofauti kabisa na jinsi wanavyochukuliwa watu wenye maadili katika mataifa yenye watu wasio na furaha kama hapa kwetu Tanzania. 
Inasikitisha sana kwamba; hapa kwetu Tanzania hatujali na kuthamini watu wenye maadili wala hatuzingatii suala zima la maadili. Na hapo ndipo mgogoro wa maendeleo unapoanzia. 
Hakika nawaambia, bila kuzingatia maadili mema hatuwezi kupata maendeleo. Maendeleo ni maendeleo ya watu. Mambo mengine kama barabara, majengo mazuri; vyombo vya usafiri n.k; ni nyenzo za kusaidia kuleta maendeleo.


Ndugu Watanzania Wenzangu;
Leo tumefikia Kilele cha kampeni ya Awamu ya Kwanza ya Kuinua Maadili Kitaifa. Tunapoadhimisha kilele hiki sio kwamba tunafunga mchakato wa masuala tuliyoanza kwenye awamu hii; bali awamu hii imetuongezea mbinu zaidi, kiona mbali zaidi na wadau zaidi kwa ajili ya kuendeleza na kuimarisha Kampeni hii nchini petu.

Maadili yakipewa kipaumbele katika maisha yetu tutajenga taifa lenye Uhuru kamili. Taifa lenye uhuru Kamili ni lile lenye uwezo wa kujitegemea kiuchumi na kifikra. Tukifikia uhuru huo tutakuwa tumejenga heshima na furaha kubwa kwa watanzania wote.

Katika suala  la umuhimu wa maadili Mwanazuoni mmoja aliwahi kusema namnukuu;
“The mark of people who have high integrity is, they always do the highest quality of work in everything they do. People with high integrity realize that everything they do is a statement about who they are as a person”.

“Alama ya watu wenye maadili ya kiwango cha juu, daima wanafanyakazi zao zote kwa kiwango cha juu zaidi. Watu wenye maadili ya kiwango cha juu hutambua kwamba kila wanachofanya kinaeleza kuhusu wao walivyo” (mwisho wa tafsiri)

Kutokana na maelezo ya mwanazuoni huyo tutakubaliana kwamba; maadili yana mchango mkubwa sana katika kukuza maendeleo ya taifa. Nawasihi watanzania wenzangu, tusitafute mchawi, turudieni maadili mema.


Ndugu Washiriki wa Kampeni;
Ndugu Watanzania Wenzangu;
Mabibi na Mabwana;
Kwa kuwa suala la maadili ni la siku hadi siku na kizazi hadi kizazi; tunaahidi kukutana tena mwaka 2019 kutoa mrejesho wa mafanikio ya kampeni ya awamu kwanza, na kutangaza awamu ya pili ya kampeni ambayo italenga mikakati madhubuti zaidi ya kulifanya suala la maadili kuwa kipaumbele cha kuboresha maisha ya Watanzania. Tunamuomba Mwenyezi Mungu mwenye Maadili yote awe msimamizi mkuu wa Kampeni hii hivyo atulinde na kutuwezesha ili Kampeni hii ishiriki kujenga mfumo hai wa Taifa letu Tanzania.

“Maadili mema na mfumo bora katika jamii yetu; vinaanza na mimi na wewe, tujielekeze kwenye ukweli huu tujenge maisha yenye tija!”

Mungu bariki mchakato wa Kampeni hii.
Mungu bariki mchakato wa kujenga mfumo hai.
Mungu ibariki Tanzania.

Asanteni kwa kunisikiliza!

Mayrose Kavura Majinge,
Kiongozi wa Kampeni ya Kuinua Maadili Kitaifa
Email: mayrosekm@gmail.com 
Temblea: www.maadilikitaifa.blogspot.com

No comments:

Post a Comment